MR Blue ni moja ya vichwa vikali kwenye Tasnia ya Muziki wa Hip Hop Bongo. Jamaa anajua sana, kwa sasa anatamba na ngoma yake ya Baki Na Mimi, amekaa kwenye gemu kwa muda mrefu bila kuchuja, sasa ni zaidi ya miaka 13, ambapo anasema ndiyo kwanza anaanza maana kuna vitu vizuri vingi amepanga kufanya katika muziki wake.
Hivi karibuni akifanya mahojiano na Showbiz, Mr Blue a.k.a Byser ambaye jina lake kamili anaitwa Herry Samir alikuwa na mengi ya kufunguka, ungana name kwenye mahojiano niliyofanya naye juzikati.
Showbiz: Habari ya mjini kwa sasa ni tamasha ambalo unakwenda kulifanya hivi karibuni Afrika Kusini, ishu hiyo imekaaje mazee?
Mr Blue: Yap ni kweli wikiendi hii (kesho kutwa) nitakuwa kwenye tamasha pale Cape Town, Afrika Kusini na baadaye nitafanya Durban.
Matamasha haya yameandaliwa na mapromota wanaofuatilia muziki wangu kutoka Nigeria, ‘so’ nashukuru sana kwa sapoti ya Watanzania ambao wamefanya muziki wangu kuendelea kukua kila siku.
Showbiz: Mchongo kwa sasa ni ishu ya wewe kugonga kolabo na mchizi kutoka Kenya, Prezzo, unafikiri nini kimechangia jamaa akaona wewe ni kati ya vichwa vya Kibongo kufanya nao kazi?
Mr Blue: Ishu kubwa ni uwezo wangu. Lakini pia Prezzo amekuwa mshkaji wangu wa karibu kwa muda mrefu na kila mara tulikuwa tunapanga kufanya kazi bila mafanikio maana mimi nilikuwa nikienda Kenya tunapishana na yeye akija Bongo tunapishana.
Safari hii alipokuja alinitafuta, tukakutana na kufanya kazi ambayo bila shaka ataiachia muda si mrefu tukimaliza ‘kushoot’ video Kenya.
Showbiz: Kuna jambo linawachanganya sana mashabiki wa muziki, hivi ni kweli BOB na Micharazo ni makundi mawili tofauti?
Mr Blue: Yaa ni kweli. Hayo ni makundi mawili tofauti lakini yanafanya kazi kwa ukaribu sana.
BOB ni kundi linalomilikiwa na mshkaji wangu wa karibu sana Nyandu Tozi na Micharazo naimiliki mimi.
Showbiz: Kwa sasa wasanii wa muziki mnakunja sana mtonyo kupitia mitandao, wewe kwa mwezi
unakunja kama ngapi hivi?
Mr Blue: Dah, hiyo ishu huwa sipendi sana kuizungumzia lakini kwa kifupi ni kwamba kupitia itandao miwili ambayo ninafanya nayo biashara, iTune na Mkito naingiza kama pesa za Kitanzania zisizopungua milioni kumi.
Showbiz: Mpaka sasa umefanya albamu ngapi?
Mr Blue: Nina albamu mbili tu ambazo ni Mr Blue ya mwaka 2003 na Yote Kheri niliyotoa mwaka 2006.
Showbiz: Tofauti na Prezzo kuna kazi yoyote uliyoifanya hivi karibuni na msanii wa nje au umepanga kufanya?
Mr Blue: Yaa mipango ipo ya kufanya kazi, hasa mtu ‘niliyemtageti’ ni nyota kutoka Nigeria, WizKid, mshkaji ninamkubali sana na ni lazima siku moja nitoke naye.
Showbiz: Swali la kizushi tu kwako, umewahi kutoka na wanawake wangapi maarufu Bongo?
Mr Blue: Dah! Mshkaji wangu, hii ishu sitapenda kuizungumzia sana kiundani kwa sababu kwa sasa nina familia. Lakini wanawake ambao wanafahamika kwa kila mmoja niliowahi kutoka nao ni Wema Sepetu na Najima.
Showbiz: Umegusia familia, kwa sasa una watoto wangapi?
Mr Blue: Wapo wawili, Kheri na Khairriya, mama yao anaitwa Wahida Mohammed, nilikutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 2004 tukiwa klabu. Baada ya kuwa washkaji wa muda mrefu, baadaye wapenzi na sasa ndiye mama wa watoto wangu.
Showbiz: Umeshawahi kupata tuzo yoyote kutoka nje?
Mr Blue: Sina tuzo yoyote kubwa kutoka nje.
Showbiz: Nakushukuru sana Blue kwa ushirikiano wako, labda kama una lolote kwa wapenzi wa kazi zako, uwafungukie.
Mr Blue: Nawashukuru kwa sapoti yao tangu mwanzo mpaka sasa, nina zaidi ya miaka kumi na tatu kwenye gemu, niwaahidi tu kuendelea kuwafanyia mambo mazuri bila shaka ziara yangu ya kwenda kupiga shoo Afrika Kusini itaambatana na vitu vipya.
Chanzo: GPL