Utabiri: Mgombea Urais kufa akitafuta urais 2015


Mrithi wa Mnajimu na Mtabiri wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Marehemu Sheikh Yahya Hussein, Alhaj Maalim Hassan Yahya Hussein, ametabiri kwamba kiongozi mmoja mzee aliye kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais, atadondoka ghafla kwenye jukwaa na kufa mwakani.

Amesema kiongozi huyo, ambaye hakumtaja jina, atafariki dunia baada ya tukio hilo wakati akikimbizwa hospitali.

Alitangaza utabiri huo, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu kutumia kwa utabiri alioutangaza mwaka 2014, uchaguzi mkuu na utabiri wa mambo mbalimbali yatakayotokea mwaka 2015.

"Kiongozi mmoja mzee kwa umri ambaye yumo kwenye sakata la urais atadondoka ghafla kwenye jukwaa na kufa akikimbizwa hospitalini," alisema Maalim Hassan.

Pia alisema kwa mwaka mpya wa 2015 kuanza siku ya Alhamisi, kunaashiria wazee maarufu na hasa wale walio katika uongozi au waliokuwa viongozi kufariki kwa wingi na kwa hilo akasema: "Mtaona ajabu yake."

Vilevile, alitabiri mwaka 2015 kwamba utakuwa wa shida kubwa kwa familia, ambazo iwapo wahusika hawatafanya juhudi za kuangalia watoto wao, vifo vya ajabu vitatokea ndani ya familia zao.

Pia alitabiri mwaka 2015, wizi utakuwa mwingi na wezi watauawa na udhalimu wa madhalimu utabainika na kuumbuka.

Aidha, alitabiri mwaka 2015 kushuhudia uongo mwingi wa kutisha hasa kutoka kwa viongozi wa kidini na kisiasa pamoja na wanawake wenye nyadhifa au maarufu katika jamii

Pia alitabiri mwaka 2015 utamweka wazi kiongozi mmoja mashuhuri wa siasa nchini kurukwa kwake kwa akili bila kufichwa au kusitiriwa kama ilivyokuwa katika mwaka 2014.

Alisema katika mwaka 2014, kiongozi huyo alikumbwa na mkasa huo, lakini suala hilo likafanywa kuwa siri kubwa.

Pia alitabiri misiba miwili ya kitaifa kutokea nchini mwaka 2015 kwa mujibu wa nyota na kwamba, kuna kiongozi mmoja wa kidini atakumbwa na kashfa ya mwaka itakayomsababishia anguko kubwa na la aibu.

Kadhalika, alitabiri viongozi wawili wa siasa na dini kwamba watakumbwa na kashfa ya ngono, ambayo itawasababishia anguko la utumishi wa kutukuka na familia zao.

Pia alitabiri mwandishi mmoja mashuhuri nchini atakumbwa na umauti wa utata utakaoitesa serikali na familia yake kutafuta suluhu.

Alisema mwaka 2015 utakuwa wa viongozi kuzama kisiasa na kukumbwa na kashfa kubwa zitakazowaondoa madarakani, ikiwa na maana kwamba viongozi wanaofahamika wataanguka kiuchumi, kisiasa, kibiashara na kijamii.


RAIS AJAYE 
Pia alitaja sifa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakayepatikana baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambazo kwa kiasi kikubwa zinamlenga Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Alisema mwenye sifa hizo, ndiye atakayekuwa Rais pekee mwenye nyota ya kudumisha sifa ya Tanzania ya amani na utulivu kwa kuwa mwaka 2015, utaanza siku ya Alhamisi, ambayo kinyota hutawaliwa na sayari ya Mushtara (Jupiter) yenye nyota za Mshale na Samaki. 

Maalim Hassan alisema Rais pekee mwenye nyota hiyo, ana sifa ya kuwa kijana mwenye mchanganyiko wa dini mbili za wazazi na/au ndoa za dini tofauti. 

"Natabiri kuwa ili Tanzania iepukane na majanga yenye dhamira ya kuifutia sifa yaje ya utulivu na amani duniani, Rais pekee mwenye nyota ya kulizuia hilo kutokea ni kijana mwenye mchanganyiko wa dini mbili za wazazi na/au ndoa za dini tofauti," alisema Maalim Hassan.

Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari walimweleza Maalim Hassan kuwa sifa hizo zinamlenga moja kwa moja January, hivyo wakataka kujua sababu za nyota kutokutaja kabisa jina la kiongozi huyo.

Akijibu swali hilo, Maalim Hassan alisema yeye hajui watu waliotangaza azma ya kutaka kugombea urais.

Alisema zaidi ya hivyo, miongoni mwa aliowasikia wakitangaza yumo pia Hamisi Andrea Kigwangallah, Mbunge wa Nzega (CCM), ambaye majina yake yanaonyesha kuwa yanatokana na dini tofauti. 

Maalim Hassan alisema atataja rasmi jina la Rais ajaye ifikapo Machi, mwakani na kwamba, kwa sasa nachokifanya ni kuonyesha mwelekeo wa kiongozi huyo mkuu mpya wa nchi. 

January, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) ni kijana mwenye umri wa miaka 41, ana mchanganyiko wa dini mbili za wazazi.

Baba yake mzazi, Yusufu Rajab Makamba ni muislamu na mama yake mzazi, Josephine ni Mkristo wa madhehebu ya Katoliki.

Maalim Hassan alisema nyota hizo za mwaka 2015 kwa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwaka huo ndiyo wa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, zinaashiria kwamba, mafanikio makubwa yatakwenda kwa vijana ambao ndiyo wenye uwezo wa kwenda kwa kasi ya nyota ya Mshale na kukabiliana na mabadiliko yanayotarajiwa kutokea.

Alisema wale watakaofanikiwa katika mwaka huo, watakuwa ni vijana ama kwa umri wao, sura zao, matendo yao au uvaaji wao.

"Kwa kuwa Tanzania imegawanyika kwenye makundi mawili ya wanaowania kiti cha urais vijana na wazee, nyota zinaonyesha kuwa watakaonufaika kinyota watakuwa ni vijana," alisema Maalim Hassan.

Hata hivyo, alisema kuna wazee pia wanaweza kufaidika, ambao ni wale watakaokuwa na sura au wenye kupenda mambo ya ujna na kusiriki kusaidia vijana.

Aliwashauri vijana wasiokuwa na sura za ujana wala kupenda au kujishughulisha na mambo ya ujana na kuonekana ni wakubwa kuliko umri wao, hao wajitambue kuwa mwaka 2015 siyo wao na ni vyema wakajiondoa mapema kupeka kuanguka na kuumbuka kwa kiwango cha hali ya juu.

Alisema kwa mujibu wa sayansi ya nyota, hali hiyo hujirudia kila baada ya kati ya miaka 50 na 55. 

"Historia inaonyesha hapa kwamba miaka 54 iliyopita Mwalimu Julius Nyerere alikuwa kijana na ndiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa kwanza wa Rais Tanzania Bara, huku wazee mashuhuri wakikubali kukaa pembeni na kuwaachia vijana kuongoza nchi.

Alitabiri mwaka 2015 nyota ya Rais Jakaya Kikwete kwamba, itazidi kung'ara kama ilivyokuwa kwa mwaka huu.

Alisema pia tishio la nchi wahisani kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi litalegezwa na kuifanya nchi kuingia kwenye uchaguzi mkuu wake kwa staha.

Alitabiri kupatwa kwa jua kwa mara ya kwanza, kutatokea Machi 20, 2015 siku ya Ijumaa.

Pia alitabiri fujo, ghasia, vifo, uadui, mauaji na usaliti mkubwa miongoni mwa wananchi na wapendwa wao kwenye uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani.

Vilevile, Jeshi la Tanzania litatumika kitaifa na kimataifa kuzima machafuko ya ndani na nje ya nchi, ambayo yatatokea na kwamba, mwaka 2015 utakuwa wa mafuriko na dhoruba vitakavyoleta madhara makubwa nchini na nje ya nchi na kushauri tahadhari kuchukuliwa kuepuka madhara hayo.
Utabiri: Mgombea Urais kufa akitafuta urais 2015 Rating: 4.5 Diposkan Oleh: Mpekuzi Huru